KWENDA HIJA
Nguzo ya tano ya Uislamu ni kwenda hija (safari kubwa ya hija). Kwa mtu mwenye uwezo, ambaye – zaidi ya mali inayotosha kuwatunza watu wa familia yake anaowaacha nyuma hadi atakaporudi – ana pesa za kutosha kwenda mji wa Makka al-Mukarrama na kurudi, ni fardhi mara moja katika umri wake, akiwa katika ihram, kufanya tawafu kuizunguka Kaaba al-Muazzama na kusimama (wuquf) katika uwanja wa Arafat, kwa sharti kwamba njia iwe salama na mwili uwe na afya.
Masharti ya hija kuwa fardhi
Kuna masharti manane ambayo ni lazima yatimie ili kwenda hija kuwe fardhi juu ya mtu: 1- Kuwa Mwislamu. 2- Kuwa baleghe. 3- Kuwa na akili. 4- Kuwa na afya. 5- Kutokuwa mtumwa. 6- Kuwa na mali iliyozidi mahitaji ya lazima. 7- Wakati wa hija uwe umefika. Wakati wa hija ni siku ya Arafa na siku nne za Idi (ya kuchinja). Muda wa safari pia unahesabiwa. 8- Kwa mwanamke aliye mbali (na Makka) kwa masafa ya safari (safar) kuwa pamoja na mumewe au na jamaa wa kiume aliye maharimu wake, ambaye ni haramu milele kufunga naye nikahi.
Kwa wanaotimiza masharti haya manane, ni fardhi kwenda hija mara moja katika umri wao. Wakienda zaidi ya mara moja, hija za miaka inayofuata ni hija za nafila. Ibada ya nafila ni ibada ambayo si fardhi wala sunna, bali inafanywa kwa hiari ya mtu mwenyewe. Thawabu ya ibada ya nafila, ikilinganishwa na thawabu ya ibada ya fardhi, ni ndogo kama tone la maji ukilinganisha na bahari. Wanazuoni wa Kiislamu hawakuwaruhusu Waislamu wanaoishi katika nchi zilizo mbali na Makka kwenda hija tena. Abdullah ad-Dahlawi (quddisa sirruhu) katika barua yake ya sitini na tatu (katika kitabu chake chenye thamani kiitwacho Makatib ash-sharifa) anasema: “Katika safari ya hija, mara nyingi haiwezekani kutekeleza ibada kikamilifu. Kwa sababu hiyo Imam Rabbani (rahmatullahi alaih), katika barua zake za 123 na 124 (katika juzuu ya kwanza ya kitabu chake kilichobarikiwa kiitwacho Maktubat), anaeleza kwamba haridhii kwenda umra wala hija ya nafila.” Hija ya nafila inayozuia kutekelezwa kwa fardhi fulani, au inayozuia wanawake kujifunika kama inavyotakiwa, ni haramu. Kwenda hija ya nafila kama hiyo, badala ya thawabu, huleta dhambi. Ni hivyo hivyo kwa kwenda umra.
Fardhi za hija
Hija ina fardhi tatu:
1- Kutia nia ya hija wakati wa kuingia katika ihram.
2- Kusimama Arafat (kisimamo kiitwacho wuquf). 3- Kufanya tawafu ya ziara (kuzunguka Kaaba).
Ni fardhi kutia nia ya kuingia katika ihram kwa ajili ya hija. Ni sunna kuvaa kipande au vipande vya kitambaa viitwavyo ihram. Ni wajibu kujiepusha na nguo zilizoshonwa.
Wakati wa kusimama Arafat ni kuanzia wakati wa zawal (jua linapopinduka, adhuhuri) siku ya tisa ya Dhul-hijja hadi asubuhi ya siku inayofuata. (Ikiwa mtu atasimama Arafat siku moja kabla au siku moja baadaye, hija huwa batili [haisihi]. Mawahabi husherehekea Idi siku moja kabla, ingawa hawajauona mwezi mwandamo. Hija ya watu wasiosimama Arafat katika wakati wake si sahihi [haisihi].)
NI WEWE, YA RASULALLAH
Kiongozi wa Mitume wote
Ni Wewe, ya Rasulallah.
Mwezi kamili wa mbingu za yakini
Ni Wewe, ya Rasulallah.
Nuru Yako ni taa ing’aayo,
Walimwengu wote wanakuhitaji Wewe,
Mwenye taji na Miraji
Ni Wewe, ya Rasulallah.
Kioo cha Rahman,
Nuru safi ya Subhan,
Siri ya al-Fatiha (as-Saba al-mathani)
Ni Wewe, ya Rasulallah.
Shahidi wa usiku wa Israa,
“Subhanalladhi asra”,
Mkusanyiko wa majina yote
Ni Wewe, ya Rasulallah.
Ewe chemchemi ya fadhila na ukarimu,
Mahali Pako ni Maqam al-Mahmud,
Makusudio ya viumbe vyote
Ni Wewe, ya Rasulallah.
Kipenzi kati ya roho zote,
Chimbuko la elimu na irfani,
Babu yangu, mwalimu wangu na sultani wangu
Ni Wewe, ya Rasulallah.
Aliyefungua njia ya tawhidi,
Aliyeifikia siri ya tafrid,
Matumaini ya Hudayi
Ni Wewe, ya Rasulallah.
Aziz Mahmud Hudayi
“Amali yenye thamani zaidi ni hija mabrur (hija iliyokubaliwa). Mwenye kufanya hija mabrur husamehewa madhambi yake. Huwa kama aliyezaliwa upya” Hadithi sharif
