Mtume Wangu Mpendwa

Dua ya mvua

Katika mwaka wa sita wa Hijra kulikuwa na ukame wa kutisha; hakuna hata tone moja lililoanguka kutoka mbinguni. Kwa sababu hii nyasi hazikuota ardhini, na watu na wanyama walipatwa na taabu ya njaa. Siku moja ya Ijumaa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, walimweleza Mtume wetu mpendwa haja yao wakisema: “Ewe Mtume wa Allah! Laiti ungeomba dua, Allahu taala atujaalie mvua!” Bwana wetu Mtume alitoka pamoja na Masahaba Wake kwenda kwenye uwanda wa wazi, na bila adhana kuadhiniwa wala ikama kusomwa, walisali sala ya rakaa mbili. Bwana wetu Mtume aliigeuza ridaa (joho) Yake iliyobarikiwa, akasema takbira. Kisha aliinua mikono Yake juu mpaka kwapa Zake zikaonekana kupitia mikono ya nguo, akaanza kuomba dua: “Ewe Allah! Tujaalie mvua!” Masahaba watukufu walikuwa wakisema: “Amin! Amin!” Wakati huo anga lilikuwa safi kabisa; hapakuwa na wingu hata moja. Bwana wetu Mtume Mtukufu alipokuwa akiomba dua, upepo ulianza kuvuma na mawingu yakaanza kufunika anga. Kisha mvua nyepesi ya manyunyu ikaanza. Safari hii Bwana wa walimwengu aliomba dua: “Ewe Allah! Inyeshe mvua hii kwa wingi kama maji yanayomwagwa kwa ndoo, na uifanye kuwa kheri kwetu!” Mara hiyo hiyo mvua ilianza kunyesha kama maji yanayomwagwa kwa ndoo. Kwenye nguo za Bwana wetu Mtume na za Masahaba watukufu hapakubaki mahali pasipolowa. Kabla hawajafika nyumbani, maji yalikuwa yamekwisha kugeuza kila mahali kuwa ziwa. Kila mtu alikuwa akitembea majini. Mvua iliendelea. Siku ile, siku iliyofuata, na iliyofuata… Wakati wa sala ya Ijumaa iliyofuata, Masahaba watukufu walisema: “Ewe Mtume wa Allah! Nyumba zetu zimeanza kuanguka kwa maji ya mvua, na wanyama wetu wameanza kuzama. Laiti ungemwomba Allahu taala mvua ikatike!” Mtume wetu mpendwa alitabasamu, akainua mikono Yake akaomba dua:

“Ewe Mola wangu! Ipeleke mvua hii mashambani, mahali panapoota miti na mabondeni!” Mara hiyo hiyo mvua iliyokuwa ikinyesha kwa wiki nzima ilikatika, na mahali palipoombewa dua pakaanza kulowa.

Walimwengu walizama katika nuru
Usiku alipozaliwa Muhammad;
Muumini na mnafiki walipambanuka
Usiku alipozaliwa Muhammad.
Nuru ilitupwa kutoka mbinguni hadi ardhini,
Wale Saba na wale Arobaini walijiunga,
Ulimi wa mtawa ulifungika
Usiku alipozaliwa Muhammad.

“Leo (katika Vita vya Ghaba) mbora wa wapanda farasi wetu ni Abu Qatada, na mbora wa askari wetu wa miguu ni Salama bin Akwa” Hadithi sharif