UTANGULIZI
Tunamhimidi (hamdu – sifa na shukrani) Allahu taala, ambaye huumba kila kiumbe hai, hukidumisha kila kilichopo katika kuwepo kila wakati, na huvilinda vyote dhidi ya hofu na kitisho. Sala (dua) na salamu zetu zimfikie Mtume Wake mpendwa Muhammad alaihis-salaam, aliye mzuri zaidi, mwema zaidi na bora zaidi wa wanadamu kwa kila hali. Sala na salamu ziwafikie Aali Zake (jamaa Zake) na ndugu Zake wanaoeneza elimu, hekima na tabia njema. Sala na salamu ziwafikie pia Masahaba1 Wake wote (radhiyallahu taala anhum – Allahu taala awe radhi nao), waliopata heshima ya kuuona uso Wake mzuri unaoponya roho na kusikia maneno Yake yenye manufaa, na kwa hiyo wakawa watu wenye thamani kubwa kuliko watu wote; na ziwafikie pia wale wanaofuata nyayo zao.
Allahu taala, kwa kuwahurumia watu wote duniani, huwaumbia na kuwapelekea mambo yenye manufaa kwao. Huko akhera, kwa ihsani Yake, Yeye2 atawasamehe waumini waliostahili kwenda Jahannam na kuwaingiza Peponi. Muhammad alaihis-salaam ni Nabii3 wa Allahu taala, Rasul (Mjumbe) Wake na Habibu (Kipenzi) Wake. Yeye ni sayyid (bwana) wa wanadamu. Wale wanaomwamini Mtume huyu mtukufu na kufuata njia Yake, hakika wamekuwa bora zaidi kuliko umma zote.
Allah Mtukufu ametuhurumia na ametujaalia neema Yake kubwa kuliko zote kwa kutufanya kuwa umma Wake (wa Muhammad alaihis-salaam).4 Ametueleza waziwazi kwamba ni lazima kumfuata na kumtii. Hata tumhimidi (hamdu) na kumshukuru Mola wetu kiasi gani kwa neema hii kubwa, bado ni kidogo. Allahu taala, kabla ya kuumba kitu chochote, aliumba nuru iliyobarikiwa ya Bwana wetu Sarwar-i alam (Bwana wa walimwengu) (sallallahu alayhi wasallam). Katika Quran tukufu Bwana wetu Mtume anaambiwa: “Tumekutuma Wewe kuwa rehema kwa walimwengu.” Na katika hadithi qudsi5 imesemwa: “Kama si Wewe, kama si Wewe, nisingeviumba viumbe!”
Sharti la msingi la imani ni “hubb fillah na bughd fillah”, yaani kuwapenda marafiki wa Allahu taala na kutowapenda maadui Zake. Bila hili hakuna ibada (kitendo cha kuabudu) inayokubaliwa – hurudishwa na kutupwa usoni mwa aliyeifanya. Kwa sababu hii, imekuwa fardhi (lazima) kwetu kumpenda “Bwana wa walimwengu”, na tumeamrishwa kuyaweka mapenzi Yake yaliyobarikiwa ndani ya nyoyo zetu na kujipamba kwa tabia Zake njema (akhlaq). Ili mapenzi haya yadumu, kwa karne nyingi vimeandikwa vitabu vinavyosimulia maisha matukufu ya Bwana wetu Mtume, na bado vinaandikwa hadi leo. Au, kwa usahihi zaidi, kupitia vitabu hivyo baraka hutafutwa kwa jina Lake tukufu. Ili nasi tupate sehemu ya baraka hii na ili nyoyo zetu zijae na kufurika mapenzi Yake, tunawashauri msome kuhusu maisha matukufu ya Sultani wa Ulimwengu, Bwana wetu Rasulullah – kazi hii imetayarishwa kwa utafiti mrefu wa vitabu vya wanazuoni wa Ahli Sunna. Allahu taala awe radhi na wote waliochangia juhudi zao humo. Allah Mtukufu azijaze nyoyo zetu sote mapenzi ya Bwana wetu Mtume na atuweke katika njia iliyonyooka waliyotufundisha wanazuoni wa Ahli Sunna! Amin.
Dr. Enver Ören
Kaaba al-Muazzama na Masjid al-Haram Makka al-Mukarrama
